MAKANISA NCHINI YAPEWA CHANGAMOTO KUONGEZA KASI YA UJENZI WA VYUO..!!!

Mkuu wa wilaya ya Singida Pascal Mabiti akifungua semina ya wahasibu wa makanisa ya Waadventista Wasabato kutoka majimbo sita ya Tanzania.

************************

Na Nathaniel Limu

Madhehebu ya dini nchini Tanzania yamehimizwa kuongeza kasi ya ujenzi wa vyuo vya walimu na vyuo vikuu, ili pamoja na mambo mengine, kuisaidia serikali kuwa na wataalam waaminifu na waadilifu katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Singida Pascal Kulwa Mabiti wakati akifungua semina ya siku tatu ambayo inamalizika leo ya wahasibu wa makanisa ya Waadventista Wasabato wa majimbo sita ya hapa nchini.

Amesema pamoja na umuhimu wa  kuwa na watumishi waaminifu na waadilifu, pia serikali ipo kwenye mapambano ya kumaliza tatizo la uhaba wa walimu, wahasibu, madaktari na wataalam mbalimbali.

Akifafanua zaidi Mabiti amesema hivi sasa serikali inao uhaba mkubwa mno wa watumishi waadilifu na waaminifu kitendo kinachochangia kukithiri kwa wizi wa raslimali za umma.

Amesema hicho ndicho kiwango cha mahitaji ya serikali ya kuwa na watu waaminifu na waadilifu hasa katika nyanja ya uhasibu,  ambako katika baadhi ya idara na taasisi za serikali, kuna ufujaji mkubwa wa fedha za umma.

Mabiti amesema kutokana na hali hiyo, upo umuhimu mkubwa kwa madhehebu ya dini kuongeza vyuo hivyo kwa imani kwamba wahitimu kutoka vyuo hivyo,pia watafunzwa kumcha Mwenyezi Mungu na kwa njia hiyo wengi watakuwa watu waaminifu na waadilifu.

Awali mshiriki wa semina hiyo Queen Kanyika, akisoma risala ya washiriki amesema madhumuni ya semina hiyo ni kukumbushana juu ya uboreshaji wa kazi ya kutunza vitabu na masuala ya utawala wa fedha.

Wahasibu kutoka majimbo sita ya makanisa ya Sabato wakihudhuria semina ya siku tatu mjini Singida. (Picha zote na Nathaniel Limu).


Mkuu wa wilaya ya Singida Pascal Mabiti (katikati) akipokelewa na Askofu wa Jimbo la Singida Pastor Maiko Rudonya na (kulia). Kushoto ni Mhazini Mkuu Kanda ya Mashariki mwa Afrika wa Kanisa la Wasabato Denis Waraha.

 
 
 

About the author

More posts by

 

 

 

Add a comment

required

required

optional