Kamanda wa polisi mkoa wa Singida,Celina Kaluba,akifunga mafunzo ya udereva kwa madereva wa pikipiki (bodaboda).Wa kwanza kushoto ni RTO mkoa wa Singida,Mrakibu msaidizi wa polisi,Mohammed Likwata.
Baadhi ya wahitumu wa mafunzo ya pikipki.
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya pikipiki, Ayubu Mahamud akitoa maelezo kwa kamanda wa polisi mkoani Singida, Celina Kaluba (wa kwanza kulia).
Mmoja wa pikipiki aliyehitimu mafunzo ya kuendesha pikipki akionyesha cheti chake.
Kamanda Celina Kaluba (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya pikipki.Kulia ni RTO, Mohammed Likwata.(Picha na Nathaniel Limu).
Na.Nathaniel Limu
Madereva wa pikipiki wanaofanya biashara ya kusafirisha abiria (bodaboda) mkoani SINGIDA,wameagizwa kuwakataa abiria wasiopenda kuvaa kofia ngumu (helment) kwa madai kwamba tabia yao hiyo, ni kinyume na sheria za usalama barabarani.
Agizo hilo limetolewa na kamanda wa polisi mkoani Singida,Celina Kaluba, wakati akifunga mafunzo ya wiki tatu ya waendeshaji zaidi ya 130 pikipiki (bodaboda) wa Singida mjini.
Amesema dereva wa bodaboda akimkataa mteja asiyependa kutumia kofia ngumu,huyo ndiye dereva mzuri anayezingatia kikamilifu sheria za barabarani.
Aidha, Kaluba amewataka wawe kioo kwa madereva wenzao ambao hawajapata mafunzo maalum ya kuendesha pikipiki kwa kutokusababisha ajali ambazo zinagharimu maisha yao na mali zao pia.
“Wimbi la ajali za bodaboda, si tu serikali inapoteza nguvu kazi na inaingia gharama kubwa ya kutibu majeruhi, bali pia ajali hizo zinachangia mno kuongeza idadi ya mayatima”,alisema kamanda huyo.
Kaluba amesema yeye binafsi amefurahishwa mno na mkakati huo wa madereva wa bodaboda kujiunga na VETA kwa ajili ya kujifunza uendeshaji bora wa pikipiki.
“Nawaahidi nyinyi wote mliohitimu mafunzo haya na kufaulu,mtapata leseni za kuendesha pikipiki zenu kupitia jeshi la polisi, ili muweze kutambuliwa kuwa ni madereva halali”Kaluba alifafanua.
Awali mwenyekiti wa umoja wa bodaboda mjinisingida, Maulid Mpondo, aliomba mafunzo hayo yawe endelevu na pia wapatiwe maeneo maalum ya kuegesha pikipiki zao.
“Mheshimiwa mgeni rasmi, tunaomba matajiri/wamiliki wa pikipiki zinazofanya shughuli ya biashara ya kusafirisha abiria, wahakikishe madereva wao wanapata mafunzo ya uendeshaji bora pikipiki pamoja na leseni,kabla ya kukabidhiwa pikipiki”alisema mwenyekiti Mpondo.












