Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mahesabu ya serikali za mitaa Mh. Idd Azzan akizungumza kwenye mkutano wa majumuisho ya ziara ya kamati hiyo mkoani Singida mwishoni mwa wiki.Kulia ni Katibu Tawala mkoa wa Singida,Liana Hassan.Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa Singida mjini.
Na.Nathaniel Limu.
Halmashauri za wilaya, manispaa na majiji nchini zimekumbushwa kuhakikisha zinafanya utafiti wa kina juu ya kupata vyanzo vipya vya mapato ili pamoja na mambo mengine, mapato ya ndani yaweze kuongezeka.
Akizungumza kwenye majumuisho ya ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyokagua baadhi ya miradi katika majimbo yote nane na mkoani Singida, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mahesabu ya Serikali ya Mitaa Mh. Idd Azzan amesema lengo la serikali ni kutaka halmashauri zote kuwa na mapato ya kukidhi mahitaji ili ziweze kujitegemea.
Amesema umakini huo wa kusimamia ukusanyaji wa mapato uende sambamba na matumizi ya fedha za umma.
Katika hatua nyingine Mh. Azzan amewataka madiwani kuongeza kasi ya kuhamasisha wananchi kuchangia maendeleo yao ili yawe endelevu.
Aidha Mh. Azzan ambaye ni mbunge wa jimbo la Kinondoni amesema upo umuhimu wa kutunga sheria ndogo zitakazosaidia wananchi kutokukwepa kuchangia maendeleo yao .
Wakati huo huo, Makamu Mwenyekti huyo amezitaka halmashauri zote nchini zilizojikopesha fedha zitokanazao na asilimia 20 ya mapato ya halmashauri, ambazo zinapashwa kulipwa kwa serikali ya vijiji, kuzirejeshwe haraka iwezekanavyo na zikabidhiwe kwa serikali za vijiji husika.








