Askari wa polisi kitengo cha usalama barabarani PC Abihudi Kasonde akitoa mada yake ya mafunzo ya sheria za usalama barabarani yaliyohudhuriwa na baadhi ya wasukuma matoroli mjini Singida.
Kamanda wa kitengo cha usalama barabarani mkoa wa Singida Mohammed Likwata akisimamia mafunzo ya sheria za usalama barabarani yaliyohudhuriwa na baadhi ya wasukuma matoroli mjini Singida.
Baadhi ya wasukuma matoroli wa mjini Singida waliohudhuria mafunzo yaliyohusu sheria za usalama barabarani. (Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Wasukuma matoroli Singida mjini wameomba watengeneza matoroli ya kubebea mizigo, kutengeneza matoroli yenye breki madhubuti, ili pamoja na mambo mengine, kuokoa maisha ya wasukuma matoroli na watumiaji wengine wa barabara.
Wasukuma matoroli hao wametoa ombi hilo wakati wakizungumza kwenye mafunzo ya siku moja yaliyohusu sheria za usalama babarani yaliyoandaliwa na jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani mkoani Singida.
Wamesema matoroli wanayotumika hivi sasa hayana breki kitendo kinachochangia kusababisha ajali na hasa sehemu zenye miteremko.
Awali askari wa usalama barabani PC Abihudi Kasonde akitoa mada yake, amewataka wasukuma matoroli wakati wote kuzingatia na kuheshimu alama na michoro iliyowekwa barabarani inayotoa taarifa, maonyo, maelezo na amri.
Amewataka pia kuacha tabia ya kubeba mizigo mikubwa inayozidi uwezo wa matoroli yao na wakati huo huo matoroli yao wayawekea ‘refleta’.
Wakati wote mnapokuwa kazini, jitahidini sana kukwepa kusababisha ajali ambazo zinaweza kuwasababishia ulemavu wa kudumu na athari zingine.










