Mbunge wa Singida Mjini Mh. Mohammed Dewji (kulia) akizungumza na waandishi wa habari jimboni kwake.
Na Jofrey Mwakibete na Nathaniel Limu.
Mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji anatarajia kutumia zaidi ya shilingi milioni 250 kuweka nyasi za bandia kwenye uwanja wa michezo wa Namfua mjini Singida.
Mh. Dewji mwanamichezo maarufu hapa nchini, amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi mdogo wa mikutano wa kanisa la katoliki mjini Singida na kuongeza kuwa shughuli hiyo ya kimaendeleo, inatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi ujao wa Julai mwaka huu.
“Tayari nyasi za bandia nimeshazinunua zipo Dar -es -salaam, kilicho mbele yangu sasa, ni kumpata mkandarasi ambaye atakisawazisha kiwanja na kuandaa mambo muhimu kwa ajili ya kutandika nyasi hizo”, amefafanua Mh. Dewji ambaye pia ni MNEC mkoa wa Singida.
Mbunge Dewji amesema wazo hilo limeungwa mkono na madiwani wa jimbo la Singida mjini katika vikao viwili alivyofanya nao katika siku mbili tofauti za ziara yake ya kikazi jimboni.
Mbunge huyo amesema anaamini hatua hiyo itawavutia vijana wengi kujitokeza kufanya mazoezi ya nguvu, katika uwanja wa Namfua ili kuibua vipaji vyao.
Kuhusu ujenzi wa kukamilisha uwanja wa Namfua, kwanza amesema kuwa hawajawahi kuahidi kumalizia ujenzi wa uwanja huo na hatarajii kufanya kazi hiyo.
“Ukamilihsaji wa uwanja wa Namfua, ahadi hiyo aliitoa mkuu wa nchi na akasema kuwa atashirikiana na mimi katika kazi hiyo, kwa hiyo sio kweli kwamba mimi binafsi nilitoa ahadi hiyo ya kumalizia ujenzi wa kiwanja cha namfua”amesema.
Amesisitiza kuwa binafsi hajawahi kuahidi kumalizia ujenzi wa uwanja wa Namfua na wala hana ndoto za kuujenga uwanja huo mali ya CCM pamoja na jengo la ofisi ya CCM mkoa.








