Mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi (katikati) akifungua mkutano wa uhamasishaji wa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa mdondo kwa kuku wa kienyeji uliofanyika mjini Singida.Wa kwanza kushoto ni mkuu wa wilaya ya Manyoni Bi.Fatuma Taufiq.
Afisa kilimo na maendeleo ya mifugo mkoa wa Singida, Dk.Martin Magagula akitoa nasaha zake kwenye mkutano wa uhamasishaji wa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa mdondo kwa kuku za kienyeji uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo ya wananchi mjini Singida.
Baadhi ya wataalam wa kilimo, mifugo na viongozi mbalimbli wa mkoa wa Singida waliohudhuria mkutano wa uhamasishaji wa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa mdondo kwa kuku wa kienyeji. (Picha zote na Nathaniel Limu).
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, imekamilisha ujenzi wa taasisi ya kutengeneza chanjo ya mifugo mjini Kibaha, kwa ajili ya kuku wa asili wa Tanzania pamoja na nchi za Afrika Mashariki.
Mkurugenzi wa Maabara kuu ya mifugo, Temeke, Dk. Sackin Das, aliyasema hayo kwenye taarifa yake inayohusu mradi wa udhibiti mdondo katika nchi za Mozambique, Malawi, Zambia na Tanzania.
Taarifa hiyo aliitoa kwenye mkutano wa uhamasishaji wa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa mdondo iliyofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Maendeleo ya wananchi (FDC) mjini Singida.
Aidha, Mkurugenzi huyo, alisema lengo la taasisi hiyo ni kutengeneza dozi milioni 100 za kutibu mdondo kwa ajili ya kuku wa asili wafugwao.
Katika hatua nyingine, Dk. Das alisema kwa sasa ugonjwa huo umetokomezwa kwenye vijiji vitano vilivyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, baada ya kufuata sheria ya uchanjiaji wa mara tatu kwa mwaka.
Alisema mradi huo wa kuzuia mdondo umefadhiliwa na serikali ya Austraia kupitia shirika la Maendeleo la Australia Agency for International Development (AusAID), pamoja na serikali ya Tanzania.
Dk.Das alisema jukumu la utekelezaji wa mradi huo limekabidhiwa kwa shirika lisilokuwa la kiserikali la Australia Kyeema Foundantion.Mradi huo unatekelezwa katika nchi nne za Malawi,Mozambique, Zambia na Tanzania kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Julai 2009 hadi Desemba mwaka huu.
Naye Ofisa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo wa mkoa wa Singida, Dk. Martin Magagura, alimwabia mkuu wa mkoa huo, Dk. Parseko Kone, kuwa kitaifa bado hawajawa na mikakati ya kuzuia ugonjwa huo.
Hata hiyo, aliipongeza Halmashauri ya wilaya ya Iramba, Halmashauri ya wilaya ya Singida, na mkoa wa Singida kwa ujumla, kwa mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo.











