Mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi akifungua warsha ya wadau wa shiriki lisilo la kiserikali la World Vision iliyofanyika kwenye ukumbi mdogo wa mikutano wa kanisa katoliki mjini Singida.Kushoto ni mratibu wa World Vision kanda ya kati,Chuma.
Mratibu wa World vision Mtinko Edwin Maleko,akitoa taarifa yake kwenye warsha ya wadau wa World vision.(Picha na Nathaniel Limu).
Na.Nathaniel Limu.
Serikali wilaya ya Singida imeahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGos) ikiwemo shirika la World vision, ili kuharakisha upatikanaji wa maendeleo endelevu kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Ahadi hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Singida Queen Mlozi, wakati akifungua warsha ya siku tatu iliyohusu kuwasilisha mpango wa STF/EMLAP unaotekelezwa na shirika la World vision.
Amesema mlango wa ofisi yake upo wazi wakati wote kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau mbali mbali wa maendeleo, katika kushirikiana kutatua kero zinazowakabili wananchi.
Mkuu huyo wa wilaya amefafanua zaidi kwa kusema, serikali kwa upande wake, haina uwezo wa kutosha kufanya kila kitu kwa maendeleo ya wananchi, kwa hiyo ushirikiano wa NGos na wadau wengine ni muhimu mno.
Katika hatua nyingine, Mlozi ametumia fursa hiyo kulipongeza shirika la World vision kwa juhudi zake za makusudi kuanzisha miradi mbali mbali wilayani Singida na hasa katika tarafa ya Mtinko.
Awali mratibu wa World vision Mtinko ADP Edwin Maleko, alisema kwa mwaka huu wametumia zaidi ya shilingi milioni 107.8 kugharamia utekelezaji wa mradi wa afya katika tarafa ya Mtinko.
Alitaja baadhi ya shughuli walizotekeleza kuwa ni kutoa mafunzo kwa vitendo kwa vikundi 51 vya lishe kuhusu njia sahihi za ulishaji wa watoto wadogo na wachanga na kugharamia kllniki tembezi 22 kwa vijiji vya Minyenye na Mughanga.
Maleko alitaja shughuli zingine kuwa ni kukarabati mtando wa maji unaohudumia vijiji vya Mtinko, Nduu, Malolo na Kijota na kuwezesha michezo ya mpira wa miguu, pete na kikapu baina ya vijana wa vijiji 19, kwa lengo la kutoa ujumbe unaohusu VVU na UKIMWI.









